Highlights

Wakaazi wa Manyatta Otte walalamika ubovu wa barabara

Na JB Nateleng

Wakaazi wa Manyatta Otte, eneo bunge la Saku, kaunti ya Marsabit, wamelalamikia ubovu wa barabara kutoka Stadium Village hadi Ajaa Tisa, wakisema hali hiyo imewaathiri pakubwa na kutatiza shughuli zao za kila siku.

Wakiongozwa na mzee Guyo Burka, pamoja na Chute Jillo wakaazi hao wamelalama changamoto kubwa ya kuwafikisha wagonjwa hospitalini kwa wakati, hasa wanawake wajawazito wanaohitaji huduma za dharura.

Wakizungumza na wanahari leo Jumatano, wakaazi hao, wameeleza kuwa wanafunzi wanakumbwa na ugumu wa kufika shuleni kwa wakati kutokana na hali mbaya ya barabara.

Pia wameibua hofu kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo mvua itaendelea kunyesha.

Kauli yao imeungwa mkono na mwenyekiti wa vijana wa Saku, Abdiaziz Boru, ambaye ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha barabara hiyo ya Manyatta Otte imekarabatiwa ili kulinda maisha na kuboresha huduma kwa wananchi.

Boru ameongeza kuwa maeneo mengi ya Marsabit ya Kati yameripoti ubovu wa barabara msimu huu wa mvua, akitoa wito kwa viongozi kuweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu.

Post Comment