Highlights

Seneta wa Marsabit aitaka serikali kuwahamisha IDPs na kushughulikia mzozo wa wakimbizi

Na Samuel Kosgei

Seneta wa Marsabit Mohamed Chute ameihimiza serikali kuu kuingilia kati haraka mzozo wa kibinadamu unaowaathiri watu waliokimbia makazi yao katika kaunti ya Marsabit pamoja na wakimbizi walioko mpakani mwa Kenya na Ethiopia.

Akizungumza katika bunge la Seneti, seneta huyo ameitaka serikali kuwahamisha na kuwafidia zaidi ya familia 500 zilizopoteza makazi yao, kujenga upya nyumba zilizoharibiwa na kurejesha maisha ya familia zilizoathirika.

Aidha, ametaka serikali kutoa kwa dharura vitambulisho vya kitaifa kwa vijana wasioweza kupata elimu na huduma za serikali kutokana na ukosefu wa stakabadhi hizo, pamoja na kuwezesha urejeshwaji wa hiari wa familia za wakimbizi katika maeneo ya mpakani kama Dilo na Magado.

Chute pia amesisitiza umuhimu wa kusaidia jamii zinazowapokea wakimbizi na kutekeleza suluhu za muda mrefu, akionya kuwa kucheleweshwa kwa hatua hizo kunaweza kuongeza ukosefu wa usawa na kuzorotesha usalama katika eneo hilo.

Post Comment