Kamishna wa Marsabit James Kamau aonya vijana dhidi ya kujihusisha katika mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi
Na JB Nateleng
Onyo limetolewa kwa vijana watakaopatikana wakijihusisha katika mahusiano ya kimapenzi au kurandaranda na wanafunzi wa shule katika kaunti ya Marsabit.
Onyo hilo limetolewa na Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, James Kamau, ambaye amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya vijana waliomaliza shule kujihusisha katika mahusiano na wanafunzi hasa wakati wa likizo, jambo ambalo linahujumu haki na ustawi wao.
Kamishna Kamau amezungumza katika warsha iliyoandaliwa na serikali ya Kaunti ya Marsabit kupitia idara ya michezo, iliyowaleta pamoja wasichana 160 kutoka maeneo bunge yote manne hapa jimboni na ambayo imefanyika katika shule ya Moi Girls, eneo bunge la Saku. Kamau ameonya dhidi ya vitendo vya kuwapeleka wanafunzi katika matembezi yasiyo rasmi, vikao vya upigaji picha pamoja na maeneo hatarishi kama misitu, wakati wanapaswa kuwa nyumbani wakisoma na kusaidia wazazi, ni kinyume cha sheria.
Kamau, amewataka wanafunzi kujiepusha na matumizi ya mihadarati, akisema kuwa dawa hizo zinapotosha maadili na kuathiri taswira yao katika jamii.
Aidha, amewahimiza wasichana walioshiriki hafla hiyo kuwa mabalozi bora katika jamii kwa kuelimisha wenzao kuhusu madhara ya ukeketaji na umuhimu wa kuukomesha kabisa.



Post Comment