Eneo la Basir laendelea kuzua utata huku waziri Murkomen akiagiza kusimamishwa kwa ujenzi unaoendelea
Na Caroline Waforo
Viongozi wa kaunti ya Marsabit wakiongozwa na Mbunge wa Moyale Profesa Guyo Jaldesa, Mbunge wa Saku Dido Raso, pamoja na mwakilishi wa wanawake Naomi Jillo Waqo wameendelea kupinga vikali ujenzi wa kituo kitakacholeta vitengo mbalimbali vya usalama pamoja katika eneo la Basir.
Viongozi hao walitoa kali hiyo wakati wa kikao cha kamati ya usalama ya bunge la kitaifa, kilichofanyika siku ya hapo jana Jumanne ambapo waziri wa usalama Kipchumba Murkomen alifika mbele ya kamati hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, mbunge wa Moyale Guyo Jaldesa alisisitiza kuwa eneo hilo la Basir lipo ndani ya eneobunge lake huku akikosoa vikali juhudi za hazina ya NG-CDF ya eneobunge la Eldas kuanzisha ujenzi wa kituo hicho cha usalama akisema hatua hiyo inakiuka sheria na mipaka ya kiutawala inayosimamia matumizi ya rasilimali za umma.
Mbunge wa Saku Dido Rasso alieleza Waziri Murkomen kuwa viongozi wa Marsabit hawapingi juhudi za kuimarisha usalama, bali wanataka taratibu sahihi zifuatwe.
Alihoji ufaafu wa hazina ya NG-CDF ya enebunge la Eldas kuhusika katika ujenzi wa kituo hicho cha usalama.
Naye mwakilishi wa wanawake Marsabit Naomi Jillo Wako aliitaka serikali kusimamisha ujenzi huo hadi utata wa mpaka huo kuangaziwa.
Kufuatia mvutano huo, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen ameagiza kusitishwa mara moja kwa ujenzi huo hadi pale kutakapofanyika mazungumzo na makubaliano kati ya pande husika.



Post Comment