Local Bulletins

BAADHI YA VIONGOZI MARSABIT WAMEPENDEKEZA MPAKA WA KENYA NA ETHIOPIA KUFUNGWA KUTOKANA NA MAUAJI YA WAKENYA.

Na Samuel Kosgei

 Viongozi mbali mbali kutoka kaunti ya Marsabit wanazidi kutoa rambirambi zao kufuatia mauaji ya watu wanane usiku wa Jumatatu tukio lililofanyika kati ya Ele-Dimtu na Forole eneobunge la North Horr.

Wa hivi punde kutoa risala zake na kukashifu mauaji hayo ya kinyama ni aliyekuwa mwaniaji wa wadhifa wa ugavana hapa Marsabit mwaka wa 2022 Pius Wario Yattani ambaye amesema kuwa mashambulizi hayo hayakufaa kuwepo iwapo serikali ingemakinika kwani sio mara ya kwanza tukio kama hilo kujiri mpakani mwa Kenya na Ethiopia.

Wario Yattani maaruu kama Ole Woyee ameitaka serikali kuchukulia kisa hicho cha mauaji kwa uzito mkubwa kwani si mara ya kwanza kujiri. Anamtaka waziri wa mambo ya ndani waziri Kithure Kindiki kulinda wananchi wa Kenya wanaoishi mpakani.

Anasema hata ikiwezekana mpaka kati ya Ethiopia na kenya ifungwe na serikali ili utulivu iweze kushuhudiwa katika mpaka huo.

Aidha Ole Woyee ameitaka serikali kuwapa wakaazi wa eneo hilo askari wa akiba NPR ili waweze kusaidia polisi kulinda jamii kwani eneo hilo la mpakani halikufaa kukosa bunduki za NPR ili kujilinda iwapo serikali italemewa.

Hayo yanajiri huku viongozi wa kaunti ya Marsabit wakiongozwa na Gavana Mohamud Ali wakifanya mazungumzo na katibu wa usalama wa kitaifa Raymond Omollo.

Katika kikao hicho imebainika kuwa hatua za dharura zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na mashambulizi yanaoshuhudiwa mara kwa mara.

Aidha viongozi hao wamekubaliana haja ya uwepo wa mazungumzo ya kuleta amani yakijumusha idara ya usalama, viongozi wa kisiasa pamoja na wananchi.

Hapo jana wawakilishi wadi kaunti ya Marsabit walishtumu idara ya usalama hapa Marsabit kwa madai ya kuzembea kazini huku wananchi wakishambuliwa kila mara siku za hivi karibuni.

Subscribe to eNewsletter