Local Bulletins

CHAMA CHA WALIMU MARSABIT CHAMKATAA WAZIRI MTEULE WA ELIMU WAKIDAI HANA UJUZI.

Na Samuel Kosgei

Muungano wa chama cha walimu KNUT tawi la Marsabit umepuuzilia mbali uteuzi wa Julius Migos Ogamba kuwa waziri wa elimu nchini ukidai kuwa hana ujuzi wala tajriba kuhusiana na masuala ya elimu.

Kulingana na katibu wa muungano huo wa walimu hapa Marsabit Rosemary Talaso ni kuwa rais William Ruto angemteua mtu mwenye ujuzi wa ualimu lakini sio wakili kama mteule Ogamba aliyependekezwa wiki jana na rais.

Kauli yake hiyo imesisitizwa na MCA mteule Saadia Araru ambaye ni mwanachama wa kamati ya elimu katika bunge la kaunti.

Saadia anasema kuwa mjuzi wa taaluma fulani anafaa kupewa kazi inayowiana na elimu.

Hata hivyo Saadia ambaye taaluma yake ni ualimu anasema kuwa nyadhifa za serikali mara nyingi ni za kisiasa na sio kufuzu kwa mtu.

Kauli zao hizo zinajiri siku mbili tu baada ya Makamu mwenyekiti wa pili wa kitaifa wa KNUT Aggrey Namisi kudai kuwa Ogamba ni mwanasheria na hana ujuzi wa kuendesha masuala ya elimu.

Aliongeza kuwa walimu wametilia shaka uwezo wa Ogamba kufanikisha mpito wa Mtaala mpya wa elimu ya Umilisi (CBC).

Hata hivyo wengine kama katibu mkuu wa kitaifa wa KNUT Collins Oyuu walikaribisha uteuzi huo.

Hata hivyo alimtahadharisha waziri huyo mteule kuwa wizara ya elimu si rahisi.

Ogamba alikuwa mgombea mwenza wa aliyekuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu katika kinyang’anyiro cha ugavana Kaunti ya Kisii wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Subscribe to eNewsletter