Local Bulletins

WANAHABARI MARSABIT WAKEMEA MASHAMBULIZI YA MAAFISA WA POLISI DHIDI YA WAANDISHI WA HABARI

Na Samuel Kosgei

Muungano wa waandishi wa habari kaunti ya Marsabit wamejiunga na wenzao kote nchini kushutumu dhulma na mashambulizi ya polisi dhidi ya waandishi wa habari wanaopeperusha taarifa.

Mwenyekiti wa muungano huo wa wanahabari Michael Kwena akizungumza na meza yetu ya habari amesema kuwa wanahabari wa hapa Marsabit wanasimama na wenzao kote nchini kukemea mashambulizi dhidi wanahabari yaliyofanyika wiki jana.

Amesema kuwa maafisa wa polisi waliowadhulumu wanahabari kaunti ya Nakuru na kwingineko wanafaa kukamatwa na kutiwa mbaroni ili kusitisha dhulma dhidi ya waandishi wa habari.

Aidha Kwena amesema kuwa siku za hivi karibu serikali imeashiria kutokuwa tayari kushirikiana na wanahabari na badala yake inajaribu kuzima sauti ya vyombo vya habari.

Anasema iwapo waandishi wa habari watapigwa vita au kukatazwa habari hiyo ni sawa na kumnyima wananchi haki ya kupokea taarifa kama inavyostahili kufanywa na vyombo huru vya habari.

Mike Kwoba ambaye ni mwanachama wa muungano huo na pia mwandishi wa habari mjini Marsabit anasema kuwa jukumu kuu la mwandishi ni kupitisha habari na taarifa pekee hivyo hana nia ya kujihusisha na vurugu au nia mbaya.

Hata hivyo Jacob Walter ambaye ni mwandishi wa taarifa za Gazeti amewataka waandishi wa habari nao kuripoti taarifa zao kwa njia ya uadilifu pasi na kupendelea upande wowote kwani huo ndio mwanzo wa majanga.

Subscribe to eNewsletter