Local Bulletins

WATU WANNE WAFARIKI HUKU WENGINE 7 WAKIJERUHIWA BAADA YA MGODI WA DABEL MOYALE KUPOROMOKA.

 Na Samuel Kosgei

Watu wanne wamefariki huku wengine saba wakijeruhiwa kufuatia kuporomoka kwa mgodi wa kuchimba dhahabu wa Hillo katika lokesheni ya Dabel kaunti ndogo ya Moyale.

Kulingana na idara ya usalama, karibia watu elfu mbili kutoka eneo hilo waliingia kwa nguvu sehemu hiyo na kuwalemea maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria katika eneo hilo lenye utata mwingi usiku wa Jumapili.

Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Marsabit Central David Saruni akizungumza na kituo hiki amesema kuwa maafisa wa polisi walizidiwa na idadi hiyo kubwa ya watu na hivyo kuamua kutotumia nguvu nyingi ili kuepuka madhara mengi.

Watu waliojeruhiwa amesema wanapokea matibabu katika hospitali kuu ya Moyale.

Saruni amewataka wakaazi wa eneo hilo kutohatarisha maisha yao kwa kuvamia eneo hilo la dhahabu kwa njia ya kihuni kwani wanahatarisha maisha yao na hata askari wanaolinda sehemu hiyo iliyopigwa marufuku na serikali.

Amewaomba wakaazi hao kusubiri taratibu zote za serikali zikamilike ili kurejesha huduma hizo za kusaka dhahabu katika eneo hilo ambalo limetajwa kuwa hatari kwa usalama.

Mwishoni mwa mwezi wa tano Watu watano walifariki na wengine wawili kujeruhiwa katika migodi hiyo tena licha kuwepo kwa marufuku hiyo iliyowekwa na aliyekuwa waziri wa Usalama Kithure Kindiki.

Subscribe to eNewsletter