Mabadiliko ya tabia nchi yaendelea kuathiri watoto Marsabit.
Na Nyabande Orwa
Mabadiliko ya tabia nchi yanaendelea kuwa changamoto kubwa kwa watoto wengi katika kaunti ya Marsabit. Haya ni kwa mujibu wa wadau waliozungumza na kituo hiki kuhusu athari za mabadiliko hayo kwa watoto wanaoishi katika maeneo kame na nusu kame nchini.
Kulingana na Afisa wa mazingira kaunti ya Marsabit, Somo Guyo, ukosefu wa maji na malisho ya mifugo unasababisha watoto wengi kukumbwa na utapiamlo. Aidha, baadhi yao hulazimika kuacha shule huku wengine wakikumbwa na ndoa za mapema kutokana na hali ngumu ya maisha.
Kwa upande wake, Waziri wa elimu Marsabit, Ambaro Abdullahi Ali, ukame umechangia wanafunzi wengi kukosa elimu ya msingi. Hata hivyo, amesema wizara yake imeweka mikakati ya kuhakikisha watoto wanaendelea kupata elimu kupitia shule zinazohudumiwa na walimu wanaohama kutoka eneo moja hadi jingine.
Wakati huo huo, Somo amesema mashirika mbalimbali ya kijamii pamoja na serikali za kaunti na ya kitaifa yanaendelea kushirikiana katika kuandaa sera za kuwalinda watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Ripoti ya UNICEF iliyotolewa wiki hii inaonyesha kuwa takriban watoto bilioni 1.1 duniani wanakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.



Post Comment