Madiwani waliohudumu miaka ya 1963-2013 Marsabit waitaka serikali kuwalipa pensheni
Na JB Nateleng
Madiwani wa zamani waliohudumu katika kaunti ya Marsabit kati ya mwaka 1963 na 2013 wameiomba serikali kuwapatia pensheni kama njia moja ya kutambua mchango wao katika uongozi na maendeleo ya taifa.
Wakizungumza na wanahabari, madiwani hao wamesema walishiriki katika mchakato wa kuandaa na kupitisha katiba ya mwaka 2010, ambayo imewanufaisha viongozi wa sasa wa kaunti, lakini wao hawajapata manufaa yoyote wakidai hali hiyo imewafanya kuhisi mchango wao haujatambuliwa.
Mmoja wa madiwani hao ambaye pia alikuwa mwakilishi wadi chini ya katiba mpya, Adan Chukulisa, amesema viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza amani na mshikamano katika kaunti ya Marsabit huku akiishukuru serikali kwa juhudi zake za kuendelea kudumisha amani katika eneo hili
Madiwani hao pia wamewahimiza vijana kujitokeza kuchukua vitambulisho vya taifa na kujisajili kama wapiga kura wakipongeza hatua ya serikali ya kuondoa mchakato wa uhakiki wa vitambulisho (vetting), wakisema wananchi wa Kaskazini mwa Kenya wana haki sawa ya kupata hati za utambulisho.
Aidha, wamesema wako tayari kufanya kampeni za kumuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao, wakidai amewakumbuka wakazi wa Marsabit kupitia uteuzi wa baadhi ya viongozi kutoka Marsabit katika serikali yake.



Post Comment