Highlights

Gavana Mohamud Ali azindua madarasa na gari la mafunzo katika chuo cha Saku VTC.

Na JB Nateleng.

Gavana wa kaunti ya Marsabit, Mohamud Ali, amezindua madarasa matatu mapya pamoja na gari la mafunzo katika chuo cha ufundi cha Saku (Saku VTC), eneo bunge la Saku.

Madarasa hayo yamejengwa na kufadhiliwa na kampuni ya moja ya mawasiliano humu nchini kupitia mpango wake wa wezesha vijana, na yatatumika kufundishia kozi za uchomeleaji vyuma au welding, upishi Pamoja na ufundi magari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana Ali amesema mradi huo utawapa wanafunzi fursa ya kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri na kujitegemea huku akiipongeza kampuni hiyo kwa ushirikiano wake na serikali ya kaunti, akibainisha kuwa kupitia mpango wa Wezesha Vijana, zaidi ya vijana 200 wamepata mafunzo na wengine tayari wameanzisha biashara zao.

Gavana Ali amewahimiza vijana wa Marsabit kujiunga na vyuo vya kiufundi, akisema serikali ya kaunti imeendelea kutoa mafunzo bila malipo ili kuwapa vijana ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuwawezesha kujitegemea.

Aidha, amesema serikali ya kaunti ina mpango wa kuajiri walimu zaidi kwa mkataba wa kudumu katika vyuo vya ufundi ili kuboresha mafunzo na kuwapa wanafunzi ujuzi unaowawezesha kushindana katika soko la ajira na kujitengenezea nafasi za kujipatia kipato.

Post Comment