County Updates

Hospitali ya Rufaa ya Marsabit Yazindua Mashine ya Kuzalisha Oksijeni

Picha Silvio Nangori

Na Silvio Nangori

Hospitali ya Rufaa ya Marsabit hii leo imezindua mashine ya kuzalisha oksijeni ambayo inaweza kuzalisha mitungi 10 ya kilo hamsini ndani ya saa 24.
Mashine hiyo ambayo imegharimu takriban milioni 20 imefadhiliwa na Shirika la Marekani la USAID.
Katika hafla hiyo hospitali ya Rufaa ya Marsabit vile vile ilizindua jengo la kusaidia katika shughuli ya utoaji na ufadhili wa Damu. (BloodBank)
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na Naibu Gavana wa kaunti ya Marsabit Solomon Gubo, John Kuntle kutoka shirika la USAID na viongozi wengine.
Kulingana na Afisa Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Marsabit Kussu Abduba ni kuwa kuwepo kwa mashine ya kuzalisha oksijeni kutasaidia pakubwa katika kuwahudumia wagonjwa si tu katika hospitali hiyo bali kaunti nzima ya Marsabit.
Kussu alisema kwamba awali hospitali hiyo ilikuwa inatumia takriban shillingi elfu mia mbili katika kujaza mitungi kumi huko kaunti ya Meru.

Kauli yake ilikaririwa zaidi na Waziri wa Afya katika kaunti ya Marsabit Grace Galmo ambaye alidokeza kwamba Shirika la Amref litasaidia katika kuhakikisha kwamba oksijeni inafikishwa katika kila wadi ya wagonjwa ili kurahisisha huduma hiyo zaidi.

Kulingana na Naibu Gavana wa kaunti ya Marsabit Solomon Gubo ni kuwa kuzinduliwa kwa miradi hiyo kunaleta usaidizi mkubwa na ambao haujawahi kushuhudiwa tena katika maeneo ya wafugaji.

Amewapongeza wafadhili kutoka USAID kwa ushirikiano mwema ambao unazidi kuzaa matunda.

Kwa upande wake afisa kutoka shirika la USAID John Kuntle alibainisha kuwa shirika hilo limetoa pia ufadhili wa mashine ya kuzalisha Oksijeni katika kaunti tano ambazo ni Kitui, Turkana, Garissa, Nandi na sasa Kaunti ya Marsabit.

Subscribe to eNewsletter