County Updates, Diocese of Marsabit, Local Bulletins

Vyombo Vya Usalama Jumanne Vilifanikiwa Kulizima Jaribio La Shambulizi Dhidi Ya Kituo Cha Polisi Cha Turbi Eneo Bunge La North Horr Katika Kaunti ya Marsabit.

Picha; Hisani

By Adano Sharawe,

Vyombo vya Usalama Jumanne vilifanikiwa kulizima jaribio la shambulizi dhidi ya Kituo cha Polisi cha Turbi eneo bunge la North Horr katika Kaunti ya Marsabit.

Hii ni kulingana na Kaimu Mkuu wa Polisi eneo la Turbi David Muthure aliyefichua kwamba watu wanne waliwafyatulia risasi maafisa wa kituo hicho.

Muthure amesema kwamba maafisa walijibu kwa haraka na kufuata watu hao hadi kwenye msitu wa Funan Idhaa, ambao wanaamini ni kambi ya mazoezi na himaya ya majambazi wanaoaminika kuhangaisha raia kwenye mpaka wa Sololo na Turbi.

Maafisa hao walifanikiwa kupata magwanda ya kijeshi, viatu, vifurushi vya nguo za raia, vyakula na vifaa vya kivita katika kambi hiyo.

Muthure amepongeza juhudi za pamoja yao maafisa wa usalama waliojibu kwa haraka na kutibua jaribio la wahalifu hao.

Kisa hicho kimejiri siku chache tu baada ya gari moja la serikali ya kaunti kunaswa na maafisa wa kushika doria katika mpaka wa Turbi-Sololo likidaiwa kuwasambazia silaha na chakula majambazi kwenye msitu wa Funan Qumbi.

Hata hivyo, wakizungumza Jumatatu Naibu Gavana wa Kaunti ya Marsabit Solomon Gubo Riwe pamoja na Waziri wa Maji Adan Kaneno, walisema kuwa gari hilo lilikuwa linawasafirisha mafundi wa maji waliokuwa kwenye ziara rasmi ya kikazi ya kukarabati visima vya maji katika maeneo ya Butiye, Obbu, Uran na Turbi.

Subscribe to eNewsletter