County Updates, Diocese of Marsabit, Local Bulletins

Asilimia 97% Ya Wanafunzi Wa Shule Za Msingi Na Asilimia 96 Ya Wale Wa Sekondari Katika Kaunti Ya Marsabit Wamerejea Shuleni – Asema Kamishna Paul Rotich.

Picha;Hisani

By Silivio Nangori,

Kamishna wa kaunti ya Marsabit Paul Rotich amewarai wazazi kuwaelekeza watoto wao katika maswala mengi za maisha na katika masomo yao ili kupunguza utovu wa nidhamu.

Akizungumza na kituo hiki Rotich amesema kwamba asilimia 97% ya wanafunzi wa shule za msingi na asilimia 96 ya wale wa sekondari wamerejea shuleni.

Kamishna Rotich vile vile amesema kwamba idadi ndogo ya wanafunzi waliorejea shuleni imechangiwa na wengi wao kushiriki kwenye sherehe za kitamaduni akionya kwamba sherehe hizo hazifai kwa vyovyote kuadhiri masomo ya wanafunzi.

Aidha ameongeza kwamba wameweka mikakati dhabiti ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wanarejea shuleni kufikia asilimia mia moja.

Ikumbukwe shule zote humu nchini zilifungwa kutokana na kuzuka kwa maambukizi ya virusi vya corona mnamo mwezi Machi mwaka huu, kabla ya kufunguliwa tena kwa awamu.

Kuhusiana na swala la utovu wa nidhamu Rotich amelaumu wazazi na jamii kwa jumla kwa visa vya kuchomwa kwa shule.

Rotich amesema maadili ya wanafunzi hao yanaanzia nyumbani kabla kufika shuleni.

Kauli yake Rotich imejiri wakati ghasia na uharibifu wa mali zilishuhudiwa kwenye baadhi ya shule za humu nchini.

 

Subscribe to eNewsletter