Viongozi wa kidini wakemea kisa cha mauaji ya mapacha Dukana, Marsabit
January 24, 2025
Na Waandishi Wetu
Mahakama ya Marsabit imeagiza kufukuliwa na kufanyiwa upasuaji, miili ya watoto mapacha waliouawa katika kijiji cha Dololo Boji kaunti ndogo ya Dukana katika kaunti ya Marsabit.
Ni agizo ambalo limetolewa na hakimu mwandamizi wa mahakama ya Marsabit, Simon Arome ambaye ameagiza shughuli hiyo kufanyika katika muda wa siku 10 zijazo ili kubaini kiini cha kifo cha watoto hao.
Arome pia ameagiza washukiwa wanne wa mauaji hayo wanaojumuisha mama ya mapacha hao Bokayo Jaro Wario, Konso Isacko Godana, Umuro Isacko Godana na Isacko Godana Adano na ambao walifikishwa mahakamani leo hii, kuzuiliwa kwa siku 14 ili kuipa idara ya usalama nafasi ya kufanya uchunguzi.
Hii ni kufuatia ombi lililowasilishwa na mkurugezi wa mashtaka ya umma,kuendelea kuwazuilia wanne hao ambapo mahakama iliridhia na kuagiza idara ya polisi kukamilisha uchunguzi wao katika muda wa siku 14 zijazo kabla ya kesi hiyo kutajwa tena Februari tarehe 4 mwaka huu.
Mahakama vile vile imeagiza mshukiwa wa kwanza Bokayo Jaro Wario kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ili kubaini umri wake na pia kupokea huduma ya matibabu wakati wowote atahitaji.
Inakisiwa kuwa mapacha hao msichana na mvulana, waliuawa na wazazi wao kwa kunyimwa hewa pindi tu walipofika nyumbani baada ya kutoka hospitalini kutokana na Imani ya kitamaduni kuwa watoto wa kwanza mapacha katika jamii ya Gabra ni ishara ya laana kwa familia.
Ni kisa na ambacho kimeendelea kulaaniwa na watu mbalimbali jimboni Marsabit.