Local Bulletins

Wakaazi wa Loglogo waendeleza juhudi za kuondoa miti sumbufu ya Mathenge.

NA HENRY KHOYAN

 Wakaazi wa eneo la Manyatta Juu, Loglogo hii leo wamejitolea kukata miti inayotajwa kuwa sumbufu ya Mathenge.

Kulingana nao eneo ambalo mti huo umetanda limekuwa halina uwezo wa kukuza mimea mingine, hivyo kuathiri upatikanaji wa malisho ya mifugo yao na hivyo kuwa na athari kubwa katika maisha yao ya kila siku.

Wakaazi hao wametambua mchango wa shirika lisilo la kiserikali la NAPO katika juhudi zao kusaidia kwa kukata miti hiyo.

Hata hivyo, bado wanahofia kwani miti hiyo inaendelea kuwa tishio katika maeneo hayo.

Aidha, wakaazi hao wamesema changamoto zinazowakumba wanapokabiliana na mti huo ni ukosefu wa ujuzi wa kutosha pamoja na ukosefu wa mavazi bora ya kuvalia wanapokabiliana na mti huo wenye kero.

Wameongeza kuwa mti huo umekuwa maficho kwa wanyama hatari kama vile chui, na hivyo kuwa tishio kwa usalama wao.

Zaidi ya hayo, wakaazi hao wana wasiwasi kwamba mti huo unaweza kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, kwani wezi wanaweza kutumia maficho hayo kujificha na kutekeleza vitendo vyao viovu.

Aidha, wametoa kilio chao kwa serikali za kaunti na kitaifa kuingilia kati swala hilo.

Wamesisitiza umuhimu wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuzuia matatizo zaidi yanayoweza kujitokeza.

 

Subscribe to eNewsletter