Local Bulletins

HEMORRHAGE (PPH) NDIO CHANZO KIKUU CHA VIFO MIONGONI MWA KINA MAMA WANAPOJIFUNGUA.

Tatizo la kuvuja damu kwa wingi baada ya kujifungua miongoni mwa kina mama wajawazito, maarufu Postpartum Hemorrhage (PPH) ndio chanzo kikuu cha vifo miongoni mwa kina mama wanapojifungua.

Haya yamewekwa wazi na mshirikishi wa idara ya afya ya uzazi kaunti ya Marsabit Halakhe Jarso ambaye amezungumza na Shajara Ya Radio Jangwani kwa njia ya kipekee.

Kulingana na Halakhe visa 176 vya akina mama kuvuja damu viliripotiwa katika mwaka 2022, visa 148 katika mwaka 2023 na mwaka huu wa 2024 visa 83 vimeshuhudiwa hadi kufikia sasa.

Kutokana na visa hivyo vifo vya akina mama vilivyotokana na kuvuja damu kwa wingi ni 6 katika mwaka 2022, visa 12 katika mwaka 2023 na mwaka huu hadi kufikia mwezi huu wa octoba visa 6 vimerekodiwa.

Katika kaunti ya Marsabit Halakhe anasema kuwa asilimia kubwa ni ya wasichana walio katika umri wa miaka 14 hadi 19 kutokana na ndoa za mapema. Hii ikiweka wazi kuwa huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya mtoto wa kike leo hii ijumaa, mikakati zaidi inapaswa kuwekwa ili kulinda haki za mtoto wa kike.

Vyanzo vingine ni pamoja na akina mama wajawazito kukosa kufika hospitalini kujifungua watoto, umbali wa maeneo wanayotoka pamoja na upungufu wa raslimali mbalimbali.

Halakhe amesema kuwa vingi vya visa hivi vimerekodiwa miongoni mwa akina mama kutoka maeneo bunge ya Northhorr na Laisamis.

Kulingana na Halakhe ipo haja ya kutambua ugonjwa huo mapema na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wakati.

Ametoa wito kwa akina mama walio na ujauzito kutembelea vituo vya afya ili kupata huduma hitajika pamoja na kuhakikisha kuwa wanafika hospitalini wakati wa kujifungua.

Kadhalika anasema kuwa serikali ya kaunti ya Marsabit inawahamasisha kinana mama kuhusu umuhimu wa kutembelea vituo vya ayfa kwa matibabu pamoja na hata kuwahamasisha wahudumu wa afya wa nyanjani.

Na katika kukabiliana tatizo hilo kote nchini wizara ya afya inayoongozwa na waziri Deborah Barasa ilizinduzi mpango wa End PPH Run ili kuokoa maisha ya akina mama wajawazito.

Subscribe to eNewsletter