County Updates, Editorial, Local Bulletins, National News, Sport Bulletins

IDARA YA USALAMA KUSHIRIKIANA NA WAZEE WA JAMII KATIKA KUDUMISHA USALAMA MJINI MARSABIT.

Na Caroline Waforo & Naima Abdullahi,

Idara ya usalama mjini Marsabit itashirikiana na wazee wa jamii katika kudumisha usalama mjini.

Hili litafanikishwa kwa kuandaa mikutano ya kiusalama na wazee wa vijijini kuanzia wiki ijayo.

Akizungumza na shajara ya radio jangwani afisini mwake kaimu kamishna wa Marsabit ya kati Kepha Maribe amesema kuwa ipo haja ya wakaazi jimboni kuhamasishwa kuhusiana na umuhimu wa kuripoti visa vyovyote vya kihalifu kwa vituo vya polisi.

Visa vya wizi wa bodaboda vimeongezeka hapa mjini Marsabit ambapo baadhi ya visa hivyo haviripotiwi katika kituo cha polisi.

Kisa cha hivi punde kikiwa ni jaribio la wizi wa bodaboda katika eneo la Camp Henry hiyo jana.

Wezi wawili waliokuwa wamejihami kwa bunduki walimtishia mhudumu moja wa bodaboda pamoja na abiria wake japo jaribio hilo la wizi lilitibuka baada ya mhudumu huyo kupiga kamsa na kuvutia umma huku wezi hao wakilazimika kutoroka.

Idara hiyo ya usalama inasema kuwa kuna mpango wa kugawa mjini wa Marsabit katika sehemu mbalimbali ili kufanikisha mikakati ya kuleta usalama.

Kadhalika idara hii inaendeleza msako wa pombe haramu pamoja na mihadarati.

Subscribe to eNewsletter