Zoezi la usajili wa watu wanaoishi na ulemavu lafanyika Marsabit Central
Na Joyce Akinyi & JB Nateleng
Zoezi la usajili wa watu wanaoishi na ulemavu limefanyika katika Lokesheni ya Mountain, kaunti ndogo ya Marsabit Central.
Akizungumza na wanahabari, afisa kutoka Idara ya Afya, Godana Doti, amesema kuwa zoezi hilo linalenga kubaini idadi ya watu wanaoishi na ulemavu ili kusaidia serikali na wadau wengine kupanga vyema huduma, mipango na shughuli zinazolenga kuboresha maisha yao.
Doti amewaraia wakazi kuto waficha watu wanaoishi na ulemavu katika familia zao kuwasajili ili wapate vyeti vitakavyowawezesha kufaidika na huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali.
Aidha, Doti amesema kupitia usajili huo, maafisa wataweza kubaini aina na kiwango cha ulemavu pamoja na athari zake katika maisha ya wahusika, jambo litakalosaidia katika utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji yao.
Kwa upande wake, Daudi Joshua, ambaye ni mmoja wa waliosajiliwa katika zoezi hilo, amepongeza hatua hiyo akisema kuwa imeleta matumaini mapya kwa watu wanaoishi na ulemavu na familia zao.



Post Comment