Washikadau wataka hatua kali kukomesha dhuluma dhidi ya mtoto wa kike Marsabit
Na Nyabande Orwa
Licha ya kuwepo kwa sheria zinazoharamisha mila na desturi zilizopitwa na wakati zinazomdhulumu mtoto wa kike, visa vya ukiukaji wa haki zake bado vinaendelea kuripotiwa katika kaunti ya Marsabit.
Hayo yamesemwa na afisa mkuu katika wizara ya jinsia, utamaduni na huduma za kijamii, AnnaMaria Denge baada ya mkutano uliowakutanisha washikadau mbalimbali kujadili ripoti ya masuala ya kijinsia iliyofanywa mapema mwaka huu katika kaunti za Marsabit, Turkana, Tana River na Garissa.
Maria amesema kuwa baadhi ya mila potovu bado zinaendelea kufanyika kwa siri katika maeneo ya mashinani huku akieeleza kuwa kuna haja ya ushirikiano kati ya maafisa wanaotekeleza sheria na wananchi wa mashinani ili kuhakikisha mianya inayochangia dhuluma dhidi ya mtoto wa kike inazibwa.
Wakati huo huo, mwanaharakati wa haki za binadamu, Pricillar Kilunda, ameitaka serikali kuimarisha usimamizi wake ili kuhakikisha maafisa wa serikali kama machifu wanaacha kutatua kesi za dhuluma nje ya mfumo wa sheria.
Kilunda pia ameitaka jamii kuripoti visa vya ukatili na dhuluma kwa vyombo vya usalama ili hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake, kiongozi wa vijana Marsabit, Abdiaziz Boru, amesema kampeni za kutetea haki za mtoto wa kike zimeleta mafanikio makubwa, lakini amedai kuwa mtoto wa kiume amesahaulika katika juhudi hizo.
Boru ametoa wito kwa wadau na jamii kuhakikisha watoto wa kiume pia wanalindwa dhidi ya aina mbalimbali za dhuluma zinazoweza kuwakumba.



Post Comment