Wakazi Marsabit watakiwa kujitayarisha kwa Mvua za El Niño Mwishoni mwa 2026
Na JB Nateleng
Wakazi wa Kaunti ya Marsabit wamehimizwa kujitayarisha mapema kwa uwezekano wa mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kati ya mwezi Septemba na Desemba mwaka 2026.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Marsabit, John Nguyo, amesema utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa athari kubwa zaidi za mvua hizo zinatarajiwa kati ya Oktoba na Desemba, ambapo kiwango na marudio ya mvua vinaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Nguyo amesema hali hiyo inaweza kusababisha mafuriko ya ghafla, mito kufurika na kuathiri miundombinu katika maeneo mbalimbali ya kaunti akiongeza kuwa hatari ya mafuriko inaweza kudumu kwa kipindi cha miezi mitatu hadi minne, huku akiwataka wakazi kuepuka kuishi karibu na njia za mafuriko na maeneo ya laga yaliyowahi kushuhudia mafuriko hapo awali.
Aidha, Nguyo ametaja baadhi ya maeneo yanayoweza kuathirika zaidi na mvua hizo na kuitaka serikali kuimarisha miundombinu muhimu ili kuokoa maisha na mali wakati wa majanga.
Pia ameonya kuwa mvua za El Niño zinaweza kuharibu barabara na kuongeza hatari ya magonjwa, akihimiza serikali kuwekeza zaidi katika huduma za dharura na kuendesha kampeni za uhamasishaji kwa wananchi.
Wakati huo huo, idara ya utabiri wa hali ya hewa imetabiri kipindi kirefu cha ukame kati ya msimu wa Juni hadi Septemba 2026 almaarufu (JJAS), ambapo sehemu kubwa ya Marsabit inatarajiwa kushuhudia joto la juu kuliko wastani pamoja na kiwango kidogo cha mvua.
Kwa mujibu wa Nguyo, hali hiyo inaweza kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo pamoja na shughuli za kilimo zinazotegemea mvua.
Hata hivyo, maeneo yaliyo karibu na Mlima Marsabit na sehemu za mpakani mwa Ethiopia yanatarajiwa kupokea mvua kiasi, huku maeneo mengi ya ukanda wa chini yakibaki makavu kwa muda mrefu.



Post Comment