Serekali ya kaunti ya Marsabit kujipanga Kukabiliana na Mvua za El Niño.
Serikali ya Kaunti ya Marsabit imeanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi kijacho.
Akizungumza na wanahabari, Naibu Gavana wa Marsabit, Solomon Gubo, amesema kuwa kaunti itashirikiana na idara na taasisi husika mara baada ya kupokea taarifa kamili kuhusu hali ya hewa ili kuratibu mikakati madhubuti ya kukabiliana na mafuriko na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Gubo amesema kuwa maandalizi hayo hayakujumuishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 iliyojadiliwa hivi karibuni na Wawakilishi wa Wadi, hivyo serikali ya kaunti itaunda kamati maalum ya kuandaa mpango wa dharura wa kukabiliana na hali hiyo.
Aidha, Gubo amesema kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu, ikiwemo barabara, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila usumbufu mkubwa wakati wa msimu wa mvua.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame (NDMA) Marsabit, Guyo Golicha, amesema kuwa serikali imeweka hazina maalum itakayosaidia kukabiliana na athari zozote zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Golicha pia amewahimiza wakazi wa Marsabit kuchukua tahadhari mapema na kufuatilia taarifa rasmi kutoka kwa idara za hali ya hewa ili kujilinda dhidi ya madhara yanayoweza kutokea.



Post Comment