Watu 158,000 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na maji, Marsabit
NA JB Nateleng
Takriban watu 158,000 katika kaunti ya Marsabit wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na maji kutokana na makali ya kiangazi yanayoelendelea kushuhudiwa.
Kulingana na Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame Katika kaunti ya Marsabit Guyo Golicha, idadi hii huenda ikaongezeka zaidi iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuhakikisha upatikanaji wa chakula na maji.
Akizungumza leo Alhamisi baada ya kikao cha kamati ya kutathmini majanga katika kaunti ya Marsabit (CSG) Golicha amesema kwamba maeneo mengi katika kaunti ya Marsabit yameathirika pakubwa kufuatia kufeli kwa mvua mwaka jana.
Guyo ameelezea kuwa mamlaka ya NDMA imetoa pesa za miezi mitatu za mpango wa HSNP kuwasaidia walengwa katika kupambana na makali ya njaa.
Ameongeza kwamba wanashirikiana na serikali kuu na ile ya kaunti chini ya uongozi wake Gavana Muhamud Ali ili kupata msaada kutoka kwa mashirika zaidi.
Aidha Guyo ameonya kuwa mifugo katika baadhi ya maeneo imeanza kuripoti visa vya ugonjwa wa midomo na miguu maarufu kama Foot and Mouth hali inayoweza kuwaathiri zaidi wafugaji.
Pia ameonya kuzuka kwa ugonjwa wa kichaa miongoni mwa ngamia.
Wakati uo huo, Naibu Gavana wa Marsabit Solomon Gubo amesema kwamba serikali ya kaunti imejizatiti kuhakikisha kwamba chakula cha msaada kinawafikia wakaazi walioathirika.



Post Comment