NCIC yahamasisha amani Marsabit kupinga matamshi ya chuki.
NA Nyabande Orwa
Tume ya uwiano na utangamano nchini (NCIC) imeanza mchakato wa kuhamasisha washikadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani kwa kuepuka matamshi ya chuki, hasa kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine.
Akizungumza na wanahabari wakati wa warsha ya siku mbili inayoendelea mjini Marsabit, naibu mkurugenzi wa NCIC anayeshughulikia masuala ya sheria, Kyalo Mwengi, amesema kuwa katika zama za teknolojia, matamshi mengi ya chuki yanasambazwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii.
Mwengi amesema warsha hiyo imewaleta pamoja maafisa wa serikali, vijana na viongozi wa kidini kwa sababu ya nafasi yao muhimu katika kuhamasisha jamii kuhusu amani na mshikamano.
Wakati uo huo, Mwengi amewataka wakazi wa Marsabit kutumia maarifa waliyojifunza kuhubiri amani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kwa manufaa ya maendeleo na umoja wa kijamii.
Kwa upande wao, viongozi wa kidini wamewaonya vijana na wanasiasa wanaotumia teknolojia kuchochea migawanyiko kuacha tabia hiyo mara moja kwa ajili ya kudumisha amani.
Naye naibu mwenyekiti wa kamati ya amani ya kaunti ya Marsabit, Adan Chukulisa, ameishukuru NCIC kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yamekuja wakati muafaka kwa kaunti ambayo kwa muda mrefu imekumbwa na migogoro na kusahaulika kimaendeleo.



Post Comment