Viongozi Marsabit wadai hatua dhidi ya kutoweka kwa vijana.
NA Nyabande Orwa
Viongozi wa kaunti ya Marsabit wametoa wito kwa Rais William Ruto kuingilia kati ongezeko la visa vya vijana kutoweka kwa njia za kutatanisha.
Wakizungumza wakati wa hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa madrasa ya Dakabaricha, hafla iliyowaleta pamoja viongozi wa kaunti jirani na waziri wa madini na uchumi wa samawati, Ali Joho kama mgeni wa heshima, viongozi hao wakiongozwa na gavana Mohamud Ali wamesema kila Mkenya ana haki ya kulindwa na kusikilizwa kisheria.
Viongozi hao akiwemo Seneta Mohamed Chute na Mbunge wa Saku, Dido Raso, wamemtaka rais William Ruto kuhakikisha maafisa wa usalama wanaodaiwa kuhusika katika utekaji nyara wanawajibishwa kisheria.
Walikuwa wakirejelea kisa cha kutoweka kwa kijana wa umri wa miaka 29, Liban Boru Charfi Chute, ambaye baadaye mwili wake ulipatikana umetupwa katika eneo la Yashareh, eneo bunge la Moyale.
Wakati huo huo, Mbunge Dido Raso ameomba tume ya kuajiri walimu (TSC) kushirikiana na jamii katika kuendeleza elimu kaunti ya Marsabit.
Akigusia mvutano unaoendelea kuhusu uteuzi wa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Marsabit, Raso anasema mwalimu atakayeteuliwa lazima awe na uwezo wa kuinua hadhi ya shule hiyo ambayo imeendelea kurekodi matokeo duni katika mtihani wa KCSE.



Post Comment