Wanaume wawili wanaswa na bangi ya thamani ya shilingi 70,000 Marsabit Central
Wanaume wawili wamekamatwa wakiwa na bangi yenye thamani ya shilingi 70,000 katika eneo la Manyatta Otte lokesheni ya Nagayo kaunti ndogo ya Marsabit Central.
Wawili hao walitiwa mbaroni usiku wa kuamkia Jumapili baada ya maafisa wa polisi kufanya operesheni iliyowezesha kunaswa kwa kilo 6.5 za bangi zilizokuwa zimehifadhiwa katika shehena mbili pamoja na misokoto 113 ya bangi.
Akizungumza na Shajara, OCPD wa Marsabit Central Beethoven Gachago amesema kuwa mmoja wa waliokamatwa ni mmiliki ya nyumba iliyofanyiwa operesheni hiyo, baada ya polisi kupokea taarifa kutoka kwa wananchi.
Gachago ametoa onyo kali kwa walanguzi wa dawa za kulevya pamoja na wafanyabiashara wa pombe haramu akisema kuwa watakabiliwa vikali na mkono wa sheria, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa muhimu.
Washukiwa hao wawili, Diba Saya Ali na Yusuf Tunis Abdi wamefikishwa katika mahakama ya Marsabit leo Jumatatu mbele ya Hakimu Mkuu Mkaazi Christine Wekesa.
Wawili hao wameachiliwa kwa bondi ya shilingi 300,000 au dhamana ya pesa taslimu 200,000 kila mmoja.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 22 mwezi huu wa April.



Post Comment