Wanaume wakumbushwa kutafuta msaada wa afya ya akili Mapema.
Na Nyabande Orwa
Wanaume wametakiwa kuzungumzia changamoto wanazopitia maishani kama njia ya kusaidia kukabiliana na matatizo ya afya ya akili.
Akizungumza na kituo hiki leo asubuhi katika kipindi cha Amkia Jangwani, mwanasaikolojia katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Marsabit, Victor Karani, amesema wanaume wengi wanaopata msongo wa mawazo hushindwa kueleza yale wanayopitia, jambo linalochangia kuongezeka kwa matatizo yao.
Karani pia ametoa wito kwa jamii kuweka mikakati ya kuzuia matatizo ya afya ya akili mapema, badala ya kusubiri hali iwe mbaya ndipo watu waende hospitalini kutafuta huduma za wataalamu.
Wakati huo huo, amewahimiza wanandoa kujenga mazingira ya wazi ya mazungumzo ili waweze kusaidiana wanapokumbana na changamoto mbalimbali maishani.
Kauli yake imejiri baada ya dunia kuadhimisha mwezi wa uhamasishaji kuhusu afya ya akili ya wanaume mwezi Juni.



Post Comment