Sehemu kubwa ya Marsabit kuendelea kusalia kavu, kiasi ikipokea manyunyu wiki ya kwanza ya mwezi wa saba.
Na Samuel Kosgei
Wakazi wa Kaunti ya Marsabit wanatarajiwa kushuhudia hali ya hewa ya ukavu katika maeneo mengi ya kaunti hiyo kwa kipindi cha kuanzia Juni 30 hadi Julai 6 mwaka huu.
Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, mvua zitakuwa chache au hazitanyesha kabisa katika sehemu kubwa ya kaunti. Hata hivyo, maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Ethiopia, Mlima Marsabit, Nyanda za Juu za Sololo na Hurri Hills yanaweza kupokea mvua nyepesi za hapa na pale.
Maeneo ya Marsabit Mjini, Karare na Sagante/Jaldesa yanatarajiwa kubaki makavu, huku mvua nyepesi zikitarajiwa kunyesha katika maeneo ya Mlima Marsabit na miteremko yake.
Katika Kaunti Ndogo ya North Horr, ikiwemo North Horr, Dukana na Maikona, hali ya joto na ukavu itaendelea kutawala. Hata hivyo, baadhi ya maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Ethiopia yanaweza kushuhudia mvua nyepesi za muda mfupi.
Kwa upande wa Laisamis, Logologo, Korr na Ngurunit, hali ya hewa itakuwa ya ukavu kwa sehemu kubwa, huku Korr na Ngurunit zikitarajiwa kuwa na mawingu na ukungu wakati wa asubuhi.
Katika Kaunti Ndogo ya Moyale, maeneo mengi yatabaki makavu, lakini Sololo, Milima ya Hurri na maeneo yanayopakana na Ethiopia yanaweza kupokea mvua nyepesi za kati ya milimita moja hadi nne. Uran, Obbu na Butiye zinatarajiwa kubaki na hali ya ukavu.
Ukanda wa Ziwa Turkana, ukiwemo Loiyangalani, unatarajiwa kuendelea kuwa na hali ya joto, ukavu na upepo mkali bila kutarajiwa kupokea mvua kubwa.
Aidha, maeneo ya Kargi, South Horr na maeneo jirani yanatarajiwa kuendelea kushuhudia hali ya joto na ukavu katika kipindi chote cha utabiri huu.



Post Comment