Wananchi mpakani mwa Kenya na Ethiopia watakiwa kudumisha amani baada ya mauaji wa watu 6, Illeret
NA Caroline Waforo
Wito wa amani umetolewa kwa wananchi wanaoishi mpakani mwa Kenya na Ethiopia huku wakitakiwa kujiepusha na mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Wito huu umetolewa na kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau, kufuatia kisa cha Jumanne ambapo watu sita waliuwawa katika shambulizi la wizi wa mifugo katika eneo la Illeret kaunti ya Marsabit, na majangili wanaoripotiwa kutoka nchini Ethiopia.
Kamishna Kamau amesisitiza umuhimu wa jamii kutoka pande zote mbili kukumbatia ujirani mwema ili kuepusha machafuko.
Vilevile Kamau ameweka wazi kuwa tayari mazungumzo ya amani yameanza kati ya jamii zinazoishi pande zote mbili za mpaka, huku idara ya usalama Illeret ikitakiwa kushirikiana na wenzao kutoka Hamar, Ethiopia ili kufanikisha kurejeshwa kwa mifugo iliyoibwa.
Waathiriwa wamedai kuwa wahalifu hao walitoweka na mbuzi 1,400 na ngombe 500.


Post Comment