Highlights

Wanaharakati wa Moyale Waandamana Kutetea Haki za Wanawake na Uongozi wa Kike.

Na Abdilaziz Yusuf

Wanaharakati pamoja na baadhi ya wakazi wa Kaunti Ndogo ya Moyale leo wameandamana kwa amani kuhamasisha jamii kuheshimu haki za wanawake na kutambua nafasi yao katika uongozi.

Akizungumza na kituo hiki wakati wa maandamano hayo, mwanaharakati Pricilla Kilunda ameitaka serikali kuhakikisha viongozi wanawake wanaheshimiwa na kulindwa dhidi ya aina yoyote ya udhalilishaji na ubaguzi.

Kilunda amekemea tukio linalodaiwa kutokea eneo la Sessi wiki iliyopita, ambapo baadhi ya wazee wa jamii wanadaiwa kupinga uongozi wa chifu wa eneo hilo. Amesema madai ya wazee hao kwamba kuondolewa kwao katika nafasi za usemaji kwenye mabaraza ni dhuluma hayapaswi kutumiwa kudhalilisha au kupinga uongozi wa mwanamke.

Kwa upande wao, baadhi ya vijana wa Moyale wamewataka wazee wa jamii kuheshimu viongozi walioko madarakani, wakisisitiza kuwa tofauti za maoni hazipaswi kuwa sababu ya kumdhalilisha au kumdhoofisha kiongozi yeyote wa serikali.

Naye Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, amethibitishia kituo hiki kuwa amepokea malalamishi kuhusu suala hilo na kusema ofisi yake inaendelea kulifuatilia ili kuhakikisha sheria inafuatwa na haki inatendeka.

Post Comment