Highlights

Wanafunzi Marsabit wasifiwa kwa Kudumisha nidhamu muhula huu.

Na JB Nateleng

Mkurugenzi wa Elimu kaunti ya Marsabit William Kamugunah amewapongeza wanafunzi kwa kudumisha nidhamu na kufuata kanuni za shule katika muhula huu wa pili ambao ametaja kuwa ulikuwa umajaa msukosuko pamoja na sintofahamu kati ya walimu na wanafunzi katika baadhi ya maeneo nchini

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Muziki la Shule za Kaunti ya Marsabit katika Shule ya Upili ya Moi Girls, Kamugunah amesema hali ya utulivu iliyoshuhudiwa katika shule zote Marsabit ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi na wadau wa elimu, tofauti na baadhi ya maeneo nchini ambako visa vya migomo na vurugu vimeripotiwa.

Amewahimiza wanafunzi kutumia njia rasmi za kuwasilisha malalamishi yao badala ya kuhusika katika vitendo vinavyoweza kuvuruga masomo na kuharibu mustakabali wao wa kielimu.

Aidha, amewataka wanafunzi kutumia Tamasha la Muziki kama jukwaa la kuonyesha na kukuza vipaji vyao, akisisitiza kuwa Marsabit ina hazina kubwa ya vipaji vinavyostahili kuendelezwa.

Wakati wanafunzi wakijiandaa kwa likizo fupi ya muhula wa pili itakayoanza wiki ijayo, Kamugunah amewataka wazazi kutumia kipindi hicho kuwa karibu na watoto wao, kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo na kushiriki kikamilifu katika malezi yao badala ya kuwaachia walimu jukumu hilo pekee.

Post Comment