Walimu zaidi ya 20 wanolewa kwa elimu ya kidijitali Marsabit
Na Joyce Akinyi & JB Nateleng
Zaidi ya walimu 20 kutoka kaunti ya Marsabit wamepata mafunzo ya ujuzi wa kidijitali yanayolenga kuhakikisha kaunti ya Marsabit haiwi nyuma katika utekelezaji wa elimu ya kidijitali.
Akizungumza na Shajara ya Radio Jangwani, Waziri wa Elimu wa Kaunti ya Marsabit, Ambaro Abdullah Ali, amesema mafunzo hayo yaliandaliwa na serikali ya kaunti kwa ushirikiano na tume ya kuajiri walimu (TSC) kwa ufadhili wa Baraza la Maendeleo la Kaunti za Mipakani (FCDC) na Raspberry.
Waziri huyo anasema walimu walioshiriki wametoka katika maeneo bunge yote ya kaunti ya Marsabit ikiwa na lengo la kuhakikisha kwamba hakuna mwanafunzi atakayekosa mafunzo ya kidijitali.
Ambaro amesema kuwa mafunzo hayo ambayo yaliandaliwa mwishoni mwa wiki jana yamehusisha shule 15, zikiwemo shule mbili za upili na shule 13 za msingi, kwa lengo la kuimarisha ujumuishaji wa masomo ya kidijitali katika taasisi za elimu kote Marsabit.
Waziri Ambarro ameongeza kuwa serikali ya kaunti inaendelea kuwekeza katika teknolojia ya kidijitali ili kuendana na mahitaji ya mtaala wa umilisi (CBE) na kuhakikisha wanafunzi wanapata ujuzi unaohitajika katika karne ya 21.



Post Comment