Idara ya usajili Marsabit yakanusha madai ya vitambulisho kutolewa kwa raia wa Ethiopia.
Na Samuel Kosgei
IDARA ya Usajili wa Watu katika Kaunti ya Marsabit imekanusha madai kwamba serikali inatoa vitambulisho vya kitaifa kiholela kwa raia wa Ethiopia.
Akizungumza na Radio Jangwani, Msajili Mkuu wa Watu katika kaunti ya Marsabit, Isaac Kibet, amesema kuwa idara yake hufuata taratibu zote za kisheria katika kushughulikia maombi ya vitambulisho vya kitaifa kutoka kwa waombaji wote.
Kibet alieleza kuwa ofisi yake hushirikiana kwa karibu na machifu na wasaidizi wao ili kuthibitisha uraia wa waombaji wanaotafuta vitambulisho katika kaunti ya Marsabit.
Aliongeza kuwa madai kama hayo huibuka mara kwa mara kutokana na ukaribu wa Marsabit na taifa la Ethiopia pamoja na uhusiano wa kihistoria na kifamilia uliopo kati ya baadhi ya jamii za eneo hili na zile za nchi jirani.
Wakati huo huo, Kibet amewataka wakazi wa Marsabit ambao wamekamilisha usajili wa vitambulisho vya kitaifa kufika katika ofisi za usajili au kwa machifu na manaibu wao kuvichukua.
Alisema kuwa bado kuna idadi kubwa ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa na wenyewe licha ya kuwa tayari vimetolewa.
Aidha, alibainisha kuwa tangu kuanza kwa zoezi la utoaji wa vitambulisho vipya mwaka jana, zaidi ya Wakenya 50,000 wameandikishwa katika Kaunti hii.



Post Comment