Highlights

Wachimba dhahabu Moyale wafurahia agizo la rais la kufunguliwa kwa Mgodi wa Dabel hivi karibuni.

Na Samuel Kosgei

Muungano wa wachimba dhahabu katika Eneo Bunge la Moyale kupitia chama chao cha Moyale Artisanal Union umeeleza kufurahishwa na tangazo la Rais William Ruto la kuagiza kufunguliwa kwa migodi ya dhahabu ya Hillo baada ya mwezi mmoja.

Katibu wa muungano huo, Muktar Guracha, akizungumza na kituo hiki, amesema kuwa wachimba madini wako tayari kuanza shughuli za uchimbaji mara tu mgodi utakapofunguliwa, huku wakiahidi kuzingatia sheria na masharti yote yaliyowekwa na Wizara ya Madini pamoja na vyombo vya usalama.

Guracha amesema kuwa ingawa hadi sasa bado hawajapokea mawasiliano rasmi kutoka kwa wizara husika, wana matumaini kuwa mgodi huo utafunguliwa hivi karibuni kufuatia agizo la Rais.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Idara ya Madini katika Kaunti ya Marsabit, Joe Mugendi, amesema idara hiyo iko mbioni kukamilisha mikakati ya usalama inayohitajika ili kuzuia kuzuka tena kwa migogoro kati ya wachimba madini, hali iliyochangia kufungwa kwa migodi ya Hillo hapo awali.

Mugendi amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa utaratibu na katika mazingira salama kwa wote wanaohusika.

Post Comment