Walimu 50 wa shule za upili Marsabit wapokea mafunzo kuhusu matumizi ya akili bandia (AI)
Na JB Nateleng
Walimu 50 wa shule za upili katika kaunti ya Marsabit wamepokea mafunzo kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI), hatua inayolenga kuboresha na kurahisisha mchakato wa ufundishaji.
Walimu hao, waliotoka katika shule mbalimbali jimboni, wamenufaika na mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuwasaidia kuinua ubora wa masomo na kuongeza ufanisi darasani.
Kwa mujibu wa Joseph Kuria, mratibu wa programu maalum na mafunzo ya wanafunzi kutoka Kituo cha Elimu ya Hisabati, Sayansi na Teknolojia Barani Afrika (CEMASTEA), mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha walimu kwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yanazidi kukumbatiwa duniani.
Akizungumza na wanahabari, Kuria amesema kuwa teknolojia ya akili bandia inaleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kusaidia kurahisisha maandalizi ya masomo, kupanga kazi kwa ufanisi, na kupunguza mzigo wa kazi kwa walimu, hivyo kuongeza motisha katika ufundishaji.
Aidha, ameongeza kuwa mfumo wa elimu unaozingatia umahiri (CBE) unahitaji matumizi ya teknolojia ya kisasa kama AI ili kuimarisha utekelezaji wake na kuboresha matokeo ya wanafunzi.
Wakati huo huo, walimu waliohudhuria warsha hiyo wamepongeza hatua hiyo wakisema italeta mabadiliko katika sekta ya elimu jimboni Marsabit.
Hata hivyo, wamependekeza nyongeza ya idadi ya walimu wanaopata mafunzo hayo ili kuhakikisha wanafunzi wote katika kaunti ya Marsabit wanapata manufaa ya teknolojia kwa ufasaha.



Post Comment