Wakazi wa Marsabit watakiwa kutambua mchango wa wajane na kuwajumuisha katika maendeleo
Na JB Nateleng
Huku dunia ikiadhimisha Siku ya kimataifa ya wajane leo, wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Marsabit kuwathamini wajane na kuwajumuisha kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Wito huu umetolewa na mkurugenzi wa shirika la kijamii la Wong’on Women Initiative (WWI), Teresalba Sintian, ambaye amesema kuwa licha ya maadhimisho ya siku hii, wajane wengi bado wanakumbana na ubaguzi na kutengwa katika jamii.
Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya simu, Teresalba amesema kuwa wajane wanapaswa kutambuliwa, kuheshimiwa na kupewa nafasi sawa katika masuala ya maendeleo, akisisitiza kuwa wana haki ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa taifa kama wanajamii wengine.
Teresalba pia ameeleza masikitiko yake kuhusu baadhi ya mila na desturi zinazowatenga wajane baada ya kufiwa na waume zao akisema kuwa baadhi yao hunyanyaswa na kunyimwa haki zao, hali ambayo amedai inapaswa kukomeshwa kwa kuzingatia utu, usawa na heshima kwa kila mwanadamu.
Aidha, ameitaka serikali kutenga sehemu ya rasilimali na mapato ya umma kwa ajili ya kuwawezesha wajane kiuchumi ili waweze kujitegemea, kuhudumia familia zao na kuchangia maendeleo ya jamii.
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ni kwamba kuna zaidi ya wajane milioni 258 duniani kote, ambao wameachwa bila kuonekana, bila msaada, na bila kipimo katika jamii zetu.
Na katika dunia ya sasa mizozo ya kivita, uhamaji na mzozo wa kiafya umeachangia katika ongezeko la wanawake wajane wapya na wengine wengi ambao waume wao wamepotea au kutoweka kwa njia tatanishi jambo amblo limeifanya Umoja wa Mataifa kuadhimisha tarehe 23 Juni kama Siku ya Kimataifa ya Wajane ili kuwapa wajane sauti ma uzoefu pamoja na kuhimiza msaada wa kipekee wanaohitaji.



Post Comment