Wafungwa 28 waachiliwa huru katika gereza la Moyale, wanne wakipunguziwa hukumu
Na Caroline Waforo
Wafungwa 28 katika gereza la Moyale kaunti ya Marsabit, wameachiliwa huru huku wengine wanne wakipunguziwa vifungo vyao, katika zoezi lililofanyika Ijumaa iliyopita, kwa lengo la kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu, Hakimu Mkaazi wa Mahakama ya Marsabit, Christine Wekesa, amesema kuwa wafungwa 33 walikuwa wamezingatiwa katika zoezi hilo.
Amesema idadi kubwa ya walioachiliwa ni raia wa kigeni waliokuwa wamepatikana na hatia ya kuwa nchini kinyume cha sheria.
Hakimu Wekesa ameeleza kuwa uamuzi wa kuwaachilia wafungwa au kupunguza vifungo vyao huzingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo uzito wa kosa walilotenda, mwenendo wao wakiwa gerezani pamoja na muda waliotumikia kifungo.
Aidha, amefafanua kuwa uhuru unaotolewa kwa wafungwa hao hauondoi wajibu wao wa kuendelea kuheshimu sheria na kutekeleza masharti yoyote yanayotolewa na mahakama.
Wakati huo huo, Hakimu Wekesa amewataka washtakiwa waliowahi kuweka dhamana mahakamani kuhakikisha wanachukua fedha zao mara tu kesi zao zinapokamilika.
Amesema kuwa kwa sasa kuna karibu shilingi milioni moja ambazo bado hazijachukuliwa na wahusika wake, akionya kuwa fedha hizo zinaweza kutwaliwa na serikali.
Kadhalika, Hakimu Wekesa amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wakaazi wa Marsabit kuhusu sheria pamoja na taratibu za kufuata wanapokuwa na masuala yanayohusu mahakama.
Zoezi hilo la kupunguza idadi ya wafungwa liliongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Marsabit, Francis Rayola kwa ufadhili wa shirika la Caritas.



Post Comment