Highlights

Vyama vya ushirika vyatajwa kuwa nguzo ya maendeleo Marsabit.

Na Nyabande Orwa

Naibu Gavana wa kaunti ya Marsabit, Solomon Gubo, amewahimiza wakazi wa kaunti hii kujijengea uwezo wa kiuchumi kwa kuangazia vyanzo mbadala vya mapato badala ya kutegemea ufugaji pekee.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Marsabit, eneo bunge la Saku, Gubo amesema kuwa vyama vya ushirika vinaweza kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa kiangazi, ikiwemo kupoteza mifugo na kuongezeka kwa umasikini.

Amesema kupitia vyama hivyo, wakazi wa Marsabit wanaweza kushiriki shughuli mbalimbali za kibiashara, kuimarisha kipato chao na kukuza ushirikiano kati ya jamii tofauti.

Wakati huo huo, Naibu Gavana huyo amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia fedha za wanachama kwa uadilifu na uwazi, ili kuepusha migogoro inayoweza kuvivuruga vyama hivyo.

Aidha, amewahimiza wanachama kutoruhusu siasa kuzigawa ushirika wao, akisisitiza kuwa kila Mkenya ana haki ya kuunga mkono mrengo wa kisiasa anaouchagua bila kuathiri umoja wa wengine.

Kwa upande wake, afisa mratibu wa mpango wa umoja wa mataifa wa kusaidia ugatuzi katika ngazi ya kaunti, Dub Garbicha, amesema kuwa ukuaji wa vyama vya ushirika na shughuli za biashara umechangia maendeleo ya kiuchumi, kuimarisha umoja na kudumisha amani katika kaunti hii, hali inayochochea ustawi wa wananchi.

Radio Jangwani 106.3FM is a community radio station situated in Marsabit County broadcasting from Marsabit town. It is the brain child of the bishop of catholic diocese of Marsabit, Rt. Rev. Peter Kihara. It is established with the objective of reaching the people Marsabit diocese and Marsabit County for evangelization, Education, entertaining and disseminating information to the masses.

Post Comment