Highlights

Eneo la  Dabel,Marsabit laathirika zaidi na visa vya ugonjwa wa Surua.

Na Joyce Akinyi

Kamati ya uratibu wa majanga (CSG) katika kaunti ya Marsabit imesema visa vya ugonjwa wa surua vimeongezeka kwa kiwango kikubwa mwaka huu, huku eneo la Dabel katika kaunti ndogo ya Moyale likiwa limeathirika zaidi.

Kulingana na Ripoti ya afya iliyowasilishwa katika kikao cha kamati hiyo hii leo, kati ya Januari na Juni mwaka 2026, kaunti ya Marsabit imerekodi jumla ya visa 194 vya surua, ikilinganishwa na visa 5 pekee vilivyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, visa 193, sawa na asilimia 99.5, viliripotiwa katika kituo cha afya cha Dabel, jambo linaloonyesha kuwa mlipuko wa ugonjwa huo umejikita zaidi katika eneo hilo. Aidha, zahanati ya Waye Godha iliripoti kisa kimoja, huku hospitali ya rufaa ya Marsabit na kituo cha afya cha Walda zikisalia bila kuripoti visa vipya katika kipindi hicho.

Kamati hiyo imeeleza kuwa mlipuko wa surua ulithibitishwa katika wadi ya Dabel wakati wa kipindi cha tathmini, na kutoa wito kwa wananchi kuwapeleka watoto kupata chanjo kwa wakati na kuripoti haraka visa vinavyoshukiwa kuwa vya surua katika vituo vya afya vilivyo karibu.

Maafisa wa afya pia wamehimiza wananchi kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

Post Comment