Highlights

Mahakama ya Marsabit yatoa dhamana kwa mshukiwa wa vitisho vya kisu

Na Mwandishi wetu

Mahakama ya Marsabit leo imemwachilia kwa dhamana ya pesa taslimu ya shilingi elfu 50 au bondi ya shilingi elfu 100,000 yenye mdhamini wa kiasi sawa na hicho, mshukiwa anayekabiliwa na mashtaka ya kumtishia mwenzake kwa kisu kufuatia mzozo kati yao.

Mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Marsabit, Edward Oboge, mshukiwa Kiya Kalicha, almaarufu CBD, alishtakiwa kwa makosa matatu.

Katika shtaka la kwanza, Kalicha anatuhumiwa kuwa mnamo Julai 18, 2026, mjini Marsabit, alitoa matamshi ya vitisho na kumtishia kumdunga kisu mlalamishi Abdullahi Sheikh Ismael baada ya kuzuka kwa mzozo kati yao.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anatuhumiwa kuharibu kioo cha mbele cha gari la Abdullahi Sheikh Ismael. Shtaka la tatu linamhusisha na jaribio la kumdunga mlalamishi huyo kwa kisu.

Kalicha alikamatwa jana na kufikishwa mahakamani leo, Julai 24, 2026. Hata hivyo, alitimiza masharti ya dhamana ya fedha taslimu na kuachiliwa, huku kesi hiyo ikipangwa kutajwa tena Agosti 10, 2026.

Post Comment