Highlights

Mbunge wa Laisamis Joseph Lekuton alaani wizi wa mifugo huku akiitaka idara ya usalama kukomesha visa hivyo.

Na Samuel Kosgei

Mbunge wa Laisamis Joseph Lekuton amelaani vikali uvamizi wa hivi karibuni wa mifugo katika eneo la Gudas na kuitaka idara ya usalama kuchukua hatua za haraka huku juhudi za kurejesha mifugo iliyoibwa zikiendelea.

Mbunge huyo amesema ameshirikiana na maafisa wa usalama, viongozi wa eneo hilo pamoja na wakazi kufuatia tukio hilo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuhakikisha jamii iliyoathirika inapokea msaada unaohitajika na wahusika wa uvamizi huo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Lekuton amesema wizi huo wa mifugo haukubaliki na unahatarisha amani pamoja na maisha ya wananchi wanaotegemea ufugaji kama chanzo chao kikuu cha riziki.

Aidha, amezitaka idara za usalama kuharakisha uchunguzi na kuongeza juhudi za kufuatilia na kurejesha mifugo iliyoibwa.

Kauli ya mbunge huyo inajiri wakati maafisa wa usalama wakiendelea kufuatilia taarifa mbalimbali ili kubaini waliko wahusika na mifugo iliyoibwa. Lekuton ametoa wito kwa wananchi kudumisha utulivu na kushirikiana na vyombo vya usalama wakati juhudi za kutatua suala hilo zikiendelea.

Post Comment