Marsabit Miongoni mwa Kaunti Zitakazoathiriwa Zaidi na Mvua za El Niño
Na Samuel Kosgei
Kaunti ya Marsabit ni miongoni mwa kaunti zinazotarajiwa kushuhudia athari kubwa za mvua za El Niño katika kipindi cha Oktoba, Novemba na Desemba mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa wataalamu wa hali ya hewa na wadau mbalimbali ulioandaliwa na Idara ya Kitaifa ya Hali ya Hewa, mtaalamu wa usimamizi wa majanga Zachary Misiani amesema kuwa kaunti za Marsabit, Wajir, Mandera, Garissa, Tana River, Lamu, Kilifi pamoja na baadhi ya maeneo yanayopakana na Ziwa Victoria zinatarajiwa kuathiriwa zaidi na mvua hizo kutokana na ongezeko la joto katika Bahari ya Hindi.
Kwa upande wake, mtaalamu wa misimu ya hali ya hewa Hanna Kimani amethibitisha kuwa hali ya El Niño inatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi nchini, kutegemea kiwango cha joto kitakachoshuhudiwa katika ukanda wa pwani ya Kenya.
Kimani ameueleza mkutano huo kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa washikadau kushirikiana kwa karibu na wakurugenzi wa idara za hali ya hewa katika kaunti mbalimbali pamoja na maafisa wa kilimo na mifugo ili kuhakikisha jamii zinapata taarifa sahihi kwa wakati.
Aidha, amewataka wakulima na wafugaji kufuatilia kwa karibu taarifa za wataalamu wa hali ya hewa ili kujitayarisha mapema na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Amefafanua kuwa El Niño haimaanishi mvua nyingi pekee, bali inaweza pia kusababisha vipindi vya ukame katika baadhi ya maeneo ambayo kwa kawaida hupokea mvua za kutosha.



Post Comment