Highlights

Vikundi vya akina mama Moyale vyanufaika na kongamano la VSLA 2026

NA JB Nateleng

Zaidi ya vikundi 30 vya akina mama katika eneo la Moyale vimenufaika na maonyesho na kongamano la VSLA 2026 lililofanyika katika ukumbi wa St. Paul’s ACK mjini Moyale mwishoni mwa wiki.

Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha wanachama wa vikundi mbalimbali vya akiba na mikopo, kuwapa hamasa kuhusu uwekezaji, uongozi bora na kuimarisha utendakazi wa vikundi hivyo.

Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya kipekee, Mkurugenzi wa programu katika shirika la SND chini ya mradi wa RANGE, Mohamed Wario, amesema kongamano hilo limewezesha vikundi hivyo kupata maarifa muhimu ya kuwasaidia kuchagua viongozi bora na kuboresha usimamizi wa shughuli zao za kiuchumi akiongeza kuwa kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, jamii imepata mafunzo yatakayoiwezesha kuwekeza na kujijengea uwezo wa kujitegemea.

Naye Mratibu wa Programu katika shirika la Mercy Corps, Catherine Obude, amesema mafunzo na maonyesho hayo yatachangia kuimarisha uchumi wa wanachama wa vikundi vya VSLA na kuongeza matumaini ya maendeleo kwa watu binafsi na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, afisa kutoka shirika la Smart Regional Consultant (SRC), Barrile Korme, amesema ushirikiano unaoendelea baina ya vikundi hivi utasaidia katika kupata ujuzi wa biashara, mikopo ya kifedha na mafunzo ya uwekezaji wa kidijitali ili kuboresha maisha yao kiuchumi.

Post Comment