Highlights

Tume ya uchaguzi IEBC yamteua Moses Sunkuli kuwa kaimu mtendaji wake.

Na Samuel Kosgei

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, imemteua Moses Ledama Sunkuli kuwa Afisa Mtendaji wa muda pamoja na Katibu wa Tume, uteuzi unaoanza mara moja.

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo, IEBC imesema Sunkuli, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Operesheni za Uchaguzi katika tume hiyo, atahudumu kwa muda wa miezi sita au hadi pale mchakato wa kuajiri na kumteua Afisa Mtendaji Mkuu wa kudumu utakapokamilika.

Nafasi hiyo ilibaki wazi baada ya aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu, Marjan Hussein Marjan, kujiuzulu kufuatia makubaliano ya pande zote kusitisha huduma zake.

Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, amemshukuru Marjan kwa mchango wake tangu kuteuliwa kwake mwezi Machi mwaka elfu mbili ishirini na mbili, akisema aliongoza tume katika kipindi kigumu ambapo haikuwa na makamishna kamili hadi Julai mwaka 2025.

Hata hivyo, Marjan aliondoka afisini kufuatia shinikizo kutoka vyama vya upinzani vilivyotaka ajiuzulu kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, alionya kuwa uchaguzi huo huenda usiwe huru na wa haki iwapo Marjan angebaki madarakani.

IEBC imesema Sunkuli analeta uzoefu mkubwa pamoja na uelewa mpana wa masuala ya ndani ya tume hiyo, jambo litakalosaidia katika kuendeleza shughuli za uchaguzi.

Radio Jangwani 106.3FM is a community radio station situated in Marsabit County broadcasting from Marsabit town. It is the brain child of the bishop of catholic diocese of Marsabit, Rt. Rev. Peter Kihara. It is established with the objective of reaching the people Marsabit diocese and Marsabit County for evangelization, Education, entertaining and disseminating information to the masses.

Post Comment