Highlights

Serikali yahamasisha wafugaji Marsabit kujiunga na vyama vya ushirika

Na Nyabande Orwa

Kama njia mojawapo ya kuwawezesha na kuwaendeleza wafugaji katika Kaunti ya Marsabit, serikali ya kaunti, serikali kuu na washikadau mbalimbali wameungana kuhamasisha umuhimu wa wafugaji kujiunga na vyama vya ushirika.

Akizungumza na kituo hiki wakati wa warsha ya siku moja iliyowakutanisha maafisa kutoka Idara ya serikali ya mifugo, idara ya serikali ya vyama vya ushirika pamoja na wataalamu kutoka chuo kikuu cha Strathmore na chuo kikuu cha ushirika cha Kenya, waziri wa biashara wa kaunti ya Marsabit, Jeremy Lendany, amesema kuwa njia mojawapo ya kuinua sekta ya mifugo ni kuwaunganisha wafugaji kupitia vyama vya ushirika.

Wakati uo huo, Mkurugenzi wa Idara mpya ya mifugo, Dkt. Hasan Guyo Roba, amesema kupitia warsha hiyo, wafugaji wanaelimishwa namna ya kupata masoko ya mifugo yao nje ya nchi pamoja na mbinu bora za ufugaji na ulishaji ili mifugo yao ifikie viwango vinavyohitajika katika soko la kimataifa.

Dkt. Guyo pia amesema kuwa Kichinjio cha Kisasa cha Isiolo, kinachotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni, kitachangia kuboresha ubora wa nyama kutoka eneo la Kaskazini Mashariki, ikiwemo kaunti ya Marsabit, na hivyo kuongeza fursa za biashara.

Naye Mkurugenzi wa ushirika katika kaunti ya Marsabit, Boru Sarapana, amesema serikali ya kaunti inaendelea kuimarisha juhudi za kusajili vyama vipya vya ushirika na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga navyo.

Ameongeza kuwa kuingiliwa kwa shughuli za vyama hivyo na siasa pamoja na ukosefu wa mitaji na ufadhili ni miongoni mwa changamoto zinazochangia kudhoofika kwa vyama vya ushirika katika kaunti hii.

Hata hivyo, mfugaji kutoka kaunti ya Marsabit, Omar Kutara, ametoa wito kwa serikali kupeleka mafunzo hayo moja kwa moja kwa jamii za wafugaji, kuhamasisha wananchi kuanzisha na kuendesha vyama vyao vya ushirika badala ya kutegemea ufadhili wa nje.

Pia amesema ufisadi ni miongoni mwa mambo yanayozorotesha maendeleo ya vyama vya ushirika.

Post Comment