Serikali kutenga mabilioni kuimarisha barabara Marsabit

Na Silvio Nangori
Serikali imejitolea kuimarisha miundombinu ya barabara katika Kaunti ya Marsabit kwa kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali, hatua inayolenga kupanua usafiri, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuunganisha jamii za eneo hilo na fursa za maendeleo.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Marsabit–Segel kwa gharama ya shilingi bilioni 1.4, Segel–Maikona kwa shilingi bilioni 1.8, na Sololo–Anona–Golole–Uran ambayo imepangiwa shilingi bilioni 1.
Aidha, serikali itatumia shilingi milioni 380 kuboresha Barabara ya Loglogo–Korr–Kargi, milioni 350 kwa Barabara ya North Horr–Dukana na milioni 300 kwa Barabara ya Odda–Butte.
Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Ngurnit–Loiyangalani yenye urefu wa kilomita 50, barabara za usalama za murram kwa gharama ya shilingi milioni 100, pamoja na Barabara ya Manyatta Jillo/Gororukesa ambayo imetengewa shilingi milioni 100.
Akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa mashinani kutoka Marsabit wakiongozwa na Gavana Mohamud Mohamed, Rais William Ruto amesema kuwa ujenzi wa barabara hizo utachangia kuimarisha usalama, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, pamoja na kuongeza kasi ya biashara ya mifugo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi katika maeneo mengi ya Kaskazini mwa Kenya.



Post Comment