Seneta wa Marsabit Mohammed Chute ataka uchunguzi wa haraka kufuatia mauaji ya Liban Charfi
NA JB Nateleng
Seneta wa kaunti ya Marsabit Mohamed Chute ameitaka Wizari ya Usalama wa Kitaifa kuchunguza kifo cha Liban Boru Charfi, mwanaume aliyepatikana ameuawa katika eneo la Yashareh eneo bunge la Moyale.
Katika barua kwa Waziri Kipchumba Murkomen, Seneta Chute amesema kwamba ni sharti idara hiyo ichunguze kifo cha Charfi aliyedaiwa kutekwa nyara tarehe 25 Januari mwaka 2026 katika eneo la Oda, Moyale na watu wasiojulikana na baadae mwili wake kupatikana siku ya hapo jana Jumatano.
Katika barua hiyo ya jana Jumatano, Chute ameeleza kuwa taarifa zinaashiria kuwa Charfi alitekwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa jeshi jambo ambalo limeibua wasiwasi miongoni mwa jamii.
Kulingana naye tukio hilo linaakisi hali ya wasiwasi uliopo mpakani kutokana na utovu wa usalama unaoshuhudiwa katika eneo la Moyale huku visa vya utekaji nyara vikiendelea kuongezeka.
Seneta Chute ameitaka wizara ya Usalama kuwachukulia hatua waliohusika na mauaji hayo huku akiitaka serikali kukabiliana na changamoto za kiusalama katika eneo hilo.



Post Comment