Mtaala unaoelezea mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi wazinduliwa leo Marsabit
Na JB Nateleng
Mtaala unaolenga kutoa elimu kuhusu mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi umezinduliwa leo katika Kaunti ya Marsabit.
Hatua hii inalenga kuimarisha na kufanya rahisi kwa kwa wanafunzi kuelewa masuala ya mazingira.
Kupitia mradi huo unaofadhiliwa na shirika la Wilderness Conservation Center (WCC), jumla ya shule 25 katika kaunti ya Marsabit zitanufaika.
Kwa mujibu wa mwanzilishi wa shirika hilo, Albert Borges, mtaala huo utawasaidia wanafunzi kuelewa changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kubuni njia mbadala za kukabiliana nazo, akibainisha kuwa suala hilo limekuwa changamoto kubwa kwa wakaazi wa Marsabit.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi utaanza rasmi muhula wa pili katika shule zote 25 zilizochaguliwa, ukilenga wanafunzi wa umri wa miaka 6 hadi 16.
Naye mshauri wa mradi huo, Dkt. Evaline Wemali, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Idara ya Sayansi ya Mazingira na Elimu, amesema walimu walipewa mafunzo maalum kabla ya uzinduzi huo ili kuwawezesha kutekeleza mtaala huo kwa ufanisi.

Dkt. Wemali amesisitiza kuwa walimu ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya mradi huo, unaolenga kuwapa wanafunzi maarifa ya kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Afisa wa kukadiria Ubora wa Elimu katika Kaunti ya Marsabit, Halake Bonaya, ambaye amesema mtaala huo utawapa walimu na wanafunzi ujuzi muhimu wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.



Post Comment