Highlights

Bunge la Marsabit laidhinisha bajeti ya ziada ya bilioni 11, afya ikipewa mgao mkubwa

Na Samuel Kosgei

Bunge la Kaunti ya Marsabit limeidhinisha bajeti ya ziada ya shilingi bilioni 11 jana Jumatano.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge hilo, ambaye pia ni Mwakilishi Wadi wa Korr, Daud Tomasot, bajeti hiyo ilipitia hatua zote za kisheria kabla ya kupitishwa rasmi.

Serikali ya Kaunti ya Marsabit ilikuwa imetenga shilingi milioni 260 katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026 ili kukabiliana na athari za kiangazi. Fedha hizo zilipangwa kutumika kusambaza chakula cha msaada na maji kwa waathiriwa wa ukame.

Hata hivyo, Tomasot amesema kuwa baadhi ya miradi iliyokuwa imetengewa fedha katika wadi kadhaa huenda ikarekebishwa kulingana na mabadiliko ya hali halisi. Alitolea mfano maeneo yaliyokusudiwa kupelekewa maji, lakini sasa yamepata mvua.

Katika bajeti hiyo, asilimia 60 sawa na shilingi bilioni 6.66 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida kama mishahara, huku asilimia 40 ambayo ni shilingi bilioni 4.37 zikielekezwa kwa miradi ya maendeleo.

Idara ya Afya imepewa mgao mkubwa zaidi wa shilingi bilioni 2.39, ambapo bilioni 2.19 zitatumika kwa matumizi ya kawaida na milioni 202 kwa miradi ya maendeleo.

Idara nyingine zilizopewa mgao mkubwa ni Kilimo, Ufugaji na Uvuvi zilizotengewa shilingi bilioni 1.5, huku Idara ya Fedha ikipewa shilingi bilioni 1.2.

Post Comment