Mgogoro wa maafisa wa kliniki Marsabit waendelea, huduma za afya zikikwama.
Na Nyabande Orwa
Mvutano kati ya maafisa wa kliniki na serikali ya kaunti ya Marsabit hautamalizika hadi serikali ya kaunti itakapotia saini makubaliano ya kurejea kazini na maafisa hao. Hayo ni kulingana na katibu mkuu wa muungano wa maafisa hao kitaifa, George Gibore.
Akizungumza na wanahabari katika kaunti hii leo Jumanne, Gibore amesema maafisa hao walikuwa na matumaini ya kufikia makubaliano na kurejesha huduma za afya kwa manufaa ya wakazi, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba baada ya serikali ya kaunti kudai kuwa haina fedha za kuwalipa. Amesema maafisa hao wanadai takriban shilingi milioni 2 pekee, kiasi ambacho anaamini kaunti inaweza kulipa.
Gibore ameikosoa serikali ya kaunti kwa kushindwa kuweka kipaumbele masuala ya afya, akisema wanaoathirika zaidi ni kina mama wanaohitaji huduma za kujifungua.
Naye mweka hazina wa muungano wa maafisa wa kliniki Marsabit, Shukri Ibrahim, amesema licha ya serikali ya kaunti kudai huduma zinaendelea, wakazi wa maeneo kama Moyale wanalazimika kusafiri hadi taifa jirani ya Ethiopia kutafuta matibabu na huduma za kujifungua.
Shukri ametoa wito kwa gavana Mohamed Ibrahim kuingilia kati mgogoro huo ili kuboresha hali ya sekta ya afya katika kaunti ya Marsabit.



Post Comment